Joshua 2

Rahabu Na Wapelelezi

1 aKisha Yoshua mwana wa Nuni kwa siri akawatuma wapelelezi wawili kutoka Shitimu, akawaambia, “Nendeni mkaikague hiyo nchi, hasa Yeriko.” Kwa hiyo wakaenda na kuingia kwenye nyumba ya kahaba mmoja jina lake Rahabu na kukaa humo.

2 bMfalme wa Yeriko akaambiwa, “Tazama! Baadhi ya Waisraeli wamekuja huku usiku huu kuipeleleza nchi.” 3 cHivyo mfalme wa Yeriko akatuma huu ujumbe kwa Rahabu: “Watoe wale watu waliokujia na kuingia nyumbani mwako, kwa sababu wamekuja kuipeleleza nchi yote.”

4 dLakini huyo mwanamke alikuwa amewachukua hao watu wawili na kuwaficha. Akasema, “Naam, watu hao walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka. 5 eKulipoingia giza, wakati wa kufunga lango la mji, watu hao waliondoka. Sijui njia waliyoiendea. Wafuatilieni haraka. Huenda mkawapata.” 6 f(Lakini alikuwa amewapandisha darini akawafunika kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandika darini.) 7 gBasi hao watu wakaondoka kuwafuatilia hao wapelelezi katika njia ile inayoelekea vivuko vya Yordani, mara tu wafuatiliaji walipotoka nje, lango likafungwa.

8 hKabla wale wapelelezi hawajalala, Rahabu akawaendea huko juu darini, 9 iakawaambia, “Ninajua kuwa Bwana amewapa nchi hii na hofu kuu imetuangukia kwa sababu yenu, kiasi kwamba wote waishio katika nchi hii wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yenu. 10 jTumesikia jinsi Bwana alivyokausha maji ya Bahari ya Shamu kwa ajili yenu mlipotoka Misri, pia lile mlilowatendea Sihoni na Ogu, wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani, ambao mliwaangamiza kabisa. 11 kTuliposikia juu ya hili, mioyo yetu iliyeyuka na kila mmoja alikosa ujasiri kwa sababu yenu, kwa maana Bwana Mwenyezi Mungu wenu ni Mungu juu mbinguni na duniani chini. 12 lSasa basi, tafadhali niapieni kwa Bwana, kwamba mtaitendea hisani jamaa ya baba yangu, kwa kuwa mimi nimewatendea hisani. Nipeni ishara ya uaminifu 13 mkwamba mtayahifadhi maisha ya baba yangu na mama yangu, ndugu zangu wa kiume na wa kike, pamoja na wale wote walio wa kwao na kwamba mtatuokoa na kifo.”

14 nWale watu wakamhakikishia Rahabu, “Uhai wetu kwa uhai wenu! Ikiwa hutatoa habari ya nini tunachofanya, wakati Bwana atakapotupa nchi hii, tutawatendea kwa hisani na kwa uaminifu.”

15 oKisha akawateremsha dirishani kwa kamba, kwa kuwa nyumba yake aliyokuwa anaishi ilikuwa sehemu ya ukuta wa mji. 16 pAlikuwa amewaambia, “Nendeni vilimani ili wale wafuatiliaji wasiwapate. Jificheni huko kwa siku tatu mpaka watakaporudi, hatimaye mwende zenu.”

17 qWale watu wakamwambia, “Hiki kiapo ulichotuapisha hakitatufunga, 18 risipokuwa, hapo tutakapoingia katika nchi hii, utakuwa umefunga hii kamba nyekundu dirishani pale ulipotuteremshia na kama utakuwa umewaleta baba yako na mama yako, ndugu zako na jamaa yako yote ndani ya nyumba yako. 19 sIkiwa mtu yeyote atatoka nje ya nyumba yako akaenda mtaani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, hatutawajibika. Lakini yule ambaye atakuwa ndani pamoja nawe, kama mkono wa mtu yeyote ukiwa juu yake damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu. 20 tLakini ikiwa utatoa habari ya shughuli yetu tunayofanya, tutakuwa tumefunguliwa kutoka kwenye kiapo hiki ulichotufanya tuape.”

21Naye akajibu, “Nimekubali. Na iwe kama mnavyosema.” Kwa hiyo akaagana nao, nao wakaondoka. Yeye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.

22Walipoondoka, wakaelekea vilimani na kukaa huko siku tatu, hadi wale waliokuwa wakiwafuatilia wakawa wamewatafuta njia nzima na kurudi pasipo kuwapata. 23Ndipo wale watu wawili wakaanza kurudi. Wakashuka kutoka kule vilimani, wakavuka mto na kuja kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kumweleza kila kitu kilichowapata. 24 uWakamwambia Yoshua, “Hakika Bwana ametupa nchi yote mikononi mwetu; watu wote wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yetu.”
Copyright information for SwhKC